Monday, 28 March 2011

Tamasha la aina yake la kuhamasisha uzalendo wa nchi, limeacha kishindo kizito jijini Dar es Salaam.
Idadi kubwa ya watu waliofurika kwenye Viwanja vya Biafra, Kinondoni, Dar, ni pointi ya kwanza inayothibitisha tamasha hilo limeacha historia.

The Biggest IQ, Ijumaa Wikienda lilikuwepo kwenye tamasha hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises Ltd pamoja na Clouds Media Group na hiki ndicho kilichokuwepo;

BURUDANI
Umati mkubwa uliofika kwenye Viwanja vya Biafra, ulipagawa na burudani iliyotolewa kusindikiza tukio hilo la kihistoria kwa nchi yetu.

Bendi za African Stars International ‘Twanga Pepeta’, Stone Mayiyasika, Msondo na Sikinde, zilifanya kazi kubwa ambayo iliamsha nderemo kila kona ya uwanja.

Michezo ya sarakasi ilikuwa kivutio lakini umati ulipagawa zaidi baada ya wasanii wa Bongo Fleva kupanda kwa zamu kutoa shoo.

UMATI
Umati uliofika kwenye Viwanja vya Biafra ulitisha kwa sababu watu walikuwa ni wengi, hivyo kuandika rekodi.

Umati huo, ulivuka lengo lililokuwa limekusudiwa na waandaaji ambao dhamira yao ililenga kufikisha ujumbe kwa watu kuipenda nchi yao.

UJUMBE
Wito ni watu kuipenda nchi yao na kuachana na maneno ya baadhi ya wanasiasa kukejeli amani iliyopo nchini na kukaribisha vita.

Umati uliofika Biafra ulipata nafasi ya kusikiliza ujumbe kutoka kwa watu mbalimbali ambao walielezea umuhimu wa kila Mtanzania kuipenda nchi yao na kuacha porojo za kutaka kuigeuza nchi kama Libya ilivyo sasa.

WATU WALIVYOKUBALI UJUMBE
Mwantumu Said aliliambia gazeti hili juzi kwenye Viwanja vya Biafra kuwa, alifika kwenye eneo la tukio kwa kuvutwa na burudani lakini ujumbe alioupata umemjenga kwa kiasi kikubwa.

“Sikuwahi kupata hamasa ya kuipenda nchi yangu kama ambavyo leo (juzi) nimeipata. Naipenda sana Tanzania na kuanzia leo sitaki tena kusikia habari za vita,” alisema Mwantumu.

Modest Hamdani alisema: “Mimi nafahamu athari za vita ndiyo maana niliposikia kuhusu tamasha hili la kuhamasisha uzalendo nilikuja nikiwa na ari ya kutosha ili nione hamasa itakayokuwepo.

“Nashukuru kwamba, nikiwa hapa nimepata pia burudani, nimewaona wasanii wakubwa ambao hapo kabla nilikuwa sijawahi kuhudhuria shoo zao. Kwa kweli tunatakiwa kuipenda nchi yetu.”

Christine Paul alisema: “Shukrani za dhati pamoja na pongezi nyingi ziende kwa wadhamini. Wamefanya kitu kikubwa kwa ajili ya nchi yetu. Tunataka kuona watu wa namna hii.

“Lazima tuwe mbali na chuki za watu hasa wale wasiopenda amani kwa sababu tu ya uroho wao wa madaraka. Kwa ujumbe nilioupata leo, mimi ni mzalendo halisi na nitaipigania nchi yangu.”

No comments: